Jitambulishe (Identify Yourself)
JITAMBULISHE
Uovu kweli tumelimbikiza
Yaliyomuhimu kuyapuuza
Aushi ya wengi kuteketeza
Matendo yetu kutochunguza
Thamani yake tukaipunguza
Bila shaka katamalaki kiza
Lakini haya ni' kasababisha?
Umeokoka, uovu waelimisha
Lisilohalali kuamrisha
Wanyonge si haba wadhalilisha
We' huoni wastaajabisha?
Jalali mbona wamsambaratisha?
Habari njema uliipokea
Uka'koka pasi kuchechemea
Ukweli hukusita kutetea
Majaribuni mwovu kakemea
Hivi sasa, mbona ukapotea?
Au pia, yepi yalitokea?
Kanisani wengi 'mechanganya
Ukweli wote 'mewanyang'anya
Kwa njia moja uliwakusanya
Kwa njia Saba umewatawanya
Kapuuza na hata walokukanya
Ona sasa umejichanganya!
Japo kiza kweli katamalaki
Kwake Mola sitingiziki
Ukweli wake nitaumiliki
Neno lake halibadiliki
N'taongeza na visisitizi
Kwake ng'o sibanduki!
Ni kweli dunia yabadilika
Huu ni ukweli usopingika
Lakini je, mbona watingizika?
Yakupasa vyema kueleweka
Uovuni usije shawishika
Jitambulishe pasi kububujika!
MirieDanie
Comments
Post a Comment